Maazimio 18 muhimu ya CUF juu ya hatma ya Tanzania baada ya Desemba 18,2012.

Naibu Katibu Mkuu CUF Mh.Mtatiro(katikati) wakurugenzi wa CUF akiongea na waandishi wa Habari kuhusu maazimio ya Baraza kuu CUF Dec 2012

Naibu Katibu Mkuu CUF Mh.Mtatiro(katikati) wakurugenzi wa CUF akiongea na waandishi wa Habari kuhusu maazimio ya Baraza kuu CUF Dec 2012

Naibu Katibu Mkuu CUF Mh.Mtatiro(katikati) wakurugenzi wa CUF akiongea na waandishi wa Habari kuhusu maazimio ya Baraza kuu CUF Dec 2012MAAZIMIO YA KIKAO CHA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA CUF KILICHOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA SHAABAN MLOO BUGURUNI, DAR ES SALAAM TAREHE 17-18 DISEMBA, 2012

Baraza Kuu la Uongozi Taifa la The Civic United Front (CUF- Chama Cha Wananchi) limekutana na kufanya kikao chake cha kawaida kwa mujibu wa katiba ya chama, kikao ambacho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mhe. Prof Ibrahim Lipumba. kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Shaaban Khamis Mloo, Dar es salaam, tarehe 17-18 Disemba, 2012. katika kikao hicho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipokea, kuzijadili na kuzifanyia maamuzi agenda mbalimbali zilizowasilishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ikiwa ni pamoja na;

 1. Taarifa ya utekelezaji wa kazi  za chama kwa kipindi cha Julai-Novemba, 2012
 2. Program ya kuimarisha chama kwa mwaka 2013
 3. Taarifa ya utekelezaji kazi za waheshimiwa wabunge na wajumbe wa baraza la wawakilishi wa CUF
 4. Mapendekezo ya bajeti ya chama kwa mwaka wa fedha 2013
 5. Hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini, pamoja na masuala mengineyo yaliyojadiliwa na kufanyiwa maamuzi.

baada ya mjadala wa kina kuhusiana na agenda hizo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo;

Kuhusu taarifa ya kazi za chama kwa kipindi cha Julai-Novemba2012  na taarifa ya viongozi wa kambi za CUF bungeni na Baraza la Wawakilishi;

 1. Baraza Kuu limepokea taarifa ya kazi za chama kwa kipindi cha mwezi Julai-Novemba,2012 pamoja na taarifa za viongozi wa kambi za CUF katika bunge la Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania na katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar,  limeipongeza Kamati ya Utendaji Taifa kwa kazi iliyofanywa katika kipindi hicho.

Operesheni za chama;

 1. Baraza Kuu limepongeza kazi nzuri ya uhamasishaji na uimarishaji wa chama iliyofanywa kupitia Operesheni za chama katika Mkoa wa Dar es Salaam, Arusha, Kagera, na Kigoma na kuwaagiza viongozi wa CUF katika mikoa hiyo walinde na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa ziara hizo. Limeiagiza kamati ya utendaji taifa kuandaa Operesheni hizo kwa mkoa mingine na kuhakikisha kuwa Dira ya Mabadiliko(Vision for Change)  inawafikia Watanzania wote.

Wabunge na wawakilishi;

 1. Linazipongeza kambi za CUF bungeni na katika Baraza la Wawakilishi kwa michango yao kuimarisha chama na kuwawakilisha wananchi waliowachagua katika majimbo yao na Watanzania kwa ujumla, limewataka kuongeza kasi ya kuwatetea Watanzania wote, masikini,  wanyonge, wakulima na wafanyakazi pamoja na makundi mengine yote ya kijamii katika utendaji wao wa shughuli za kila siku.

Hatua za nidhamu;

 1. Baraza Kuu la Uongozi Taifa, baada ya kupokea taarifa ya kina ya mwanachama wake na kujiridhisha na maelezo hayo, limemvua uanachama wa CUF mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Somanga-ndumo, wilayani Kilwa Yusuf Amani Muhani kutokana na uongozi mbaya kwa wananchi wake na kuingiza kwa njia ya udanganyifu taasisi ya uhifadhi wa fukwe ya bahari (Beach Management Unit- BMU) ambayo imekuwa inaathiri ustawi wa jamii ya wakazi wa kijiji hicho bila ya ridhaa ya wakazi na wananchi wa kijiji. CUF kwa kutambua haki na wajibu wa wananchi na viongozi wake, madhumuni na malengo ya kuasisiwa kwa taasisi hii imechukua hatua hiyo ikiwa ni onyo na taadhari inayoitoa kwamba kamwe CUF na viongozi wake hawapaswi kujihusisha na vitendo vya ufisadi na ukiukwaji wa misingi ya uongozi bora.

Uteuzi wa naibu katibu mkuu zanzibar;

 1. kwa mujibu wa katiba ya CUF, Baraza Kuu limemchagua Mhe Hamad Masoud kuwa Naibu Katibu Mkuu kwa upande wa Zanzibar nafasi iliyoachwa wazi na Mhe Ismail Jussa Ladhu (muwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe), aliyeomba kuachia nafasi hiyo ili aweze kuwatumikia wananchi wa Jimbo lake na kupangiwa majukumu mengine. Baraza Kuu lilimchagua Mhe Hamad Masoud kwa kura 39 za ndio, kura moja ya hapana , na kura moja iliharibika. katika uchaguzi huo Mhe Riziki Omary Juma(MB) ambaye alipendekezwa na jina lake kufikishwa mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu alijitoa katika hatua za awali kabla wajumbe wa Baraza Kuu kupiga kura.

Uchaguzi wa chama ndani ya chama;

 1. Linatoa wito kwa wanachama wote kuitumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia ndani ya chama kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya Tawi, Kata, Jimbo, Wilaya na baadae ngazi ya Taifa kwa ratiba itakayotolewa mapema kuanzia mwezi January-Aug, 2013 kwa ngazi ya Tawi hadi Wilaya na kuhitimishwa kwa Mkutano Mkuu wa Taifa mwezi Oktoba, 2013. Wanachama wote wenye nia ya kugombea nafasi ya uongozi kwa ngazi hizo wanaombwa kujitokeza kwa wingi tuweze kujipanga mapema kwa chaguzi za mwaka 2014/15. Ni matarajio ya Baraza Kuu kwamba viongozi wote waliopo madarakani sasa watatoa fursa na haki sawa kwa wanachama wote kupata haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi wa chama chetu kwa kipindi cha mwaka 2013-2018.

Jeshi la Polisi na matukio ya vurugu na mauaji ya raia;

 1. Baraza Kuu linalaani mwenendo wa matukio ya mauaji yanayosababishwa kwa uzembe wa jeshi la polisi nchini kama ilivyotokea hivi karibu mkoani kigoma, Tegeta, Dar es salaam, RPC Mwanza, Zanzibar, na hata kuwajeruhi waandishi wa habari kwa risasi kama ilivyotokea Mkoani Kilimanjaro na Dar es salaam kabla hata ya suala la mauaji ya mwandishi wa habari mkoani Iringa marehemu Daudi Mwangosi halijapatiwa hitimisho sahihi. CUF inalaani vitendo hivi vya jeshi la polisi na matumizi ya silaha bila kuwa na uangalifu na tahadhari ya kutosha. CUF inamtaka IGP kuwachukulia hatua za haraka za kisheria na kinidhamu watendaji wote wanaohusika na vitendo hivyo na kuacha muendelezo wa tabia ya kulindana kwa maovu na kuwatisha wananchi katika maeneo yalipotokea matukio haya. Inaelezwa kuwa wananchi wa kasulu, Kigoma yalipotokea mauaji ya askari polisi, kijiji kizima kimekimbilia msituni kwa vitisho vya Jeshi la polisi. Chama cha CUF hakiungi mkono suala la wananchi kujichukulia sheria mkononi na badala yake inasisitiza utendaji wa haki kwa pande zote zinazohusika na kadhia hizo.

Mjadala wa kitaifa kushughulikia nyufa mbalimbali zinazohatarisha Amani na ustawi wa Taifa letu;

 

 1. Baraza Kuu linalaani vitendo vilivyofanywa na watu wenye dhamira mbaya kwa Taifa letu kwa kuchochea vurugu za kidini kwa kuchoma makanisa na kukinajisi kitabu kitakatifu cha Quran. CUF inatoa wito kwa viongozi wa dini wote kutokubali kwa namna yeyote ile kuwa sehemu ya chanzo cha kuiingiza nchi yetu katika mgawanyiko wa kidini na badala yake sote kwa pamoja tushirikiane kuwafanya Watanzania wote kuishi kwa amani, upendo na udugu wa kitanzania.
 2. Baraza kuu linatoa wito kwa serikali ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete kuona umuhimu wa kuandaa mjadala wa kitaifa wa kuzungumzia masuala yanayohatarisha amani na ustawi wa TAIFA LETU ikiwamo kustawi kwa dhana ya uwepo wa mfumo wa ubaguzi wa kidini nchini, si vyema hata kidogo kupuuza madai haya na kamwe hayawezi kuzimwa kwa silaha za moto na mizinga pekee kila zinapojitokeza. CUF inaamini kuwa njia pekee za kuondoa mfarakano wa kidini ni mjadala wa pamoja wenye nia ya kuwaleta Watanzania wote kuwa na misinngi itakayo jenga muafaka wa kitaifa katika suala hili. CUF kikiwa ni chama kinachopigania haki sawa kwa wote hakioni sababu ya maana inayopelekea hata DPP kuwazuilia dhamana viongozi wa kiislamu Sheikh Ponda Issa Ponda na Sheikh Farid kwa upande wa Zanzibar. Kuwazuilia dhamana kwa makosa yanayodhaminika hakuwatendei haki viongozi hawa na ni uvunjwaji wa haki za binaadamu. CUF inamtaka Mhe Rais Kikwekte kuingilia kati suala hili na kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote wanatendewa haki yao kisheria.

    kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini;

 1. Chama chetu CUF bado kinaona kuwa nchi yetu imekuwa katika matatizo makubwa ya kimfumo katika kuasisi asasi zitakazojenga demokrasia na kuendeleza uchumi wa kisasa utakaoleta neema kwa wananchi wote ikilinganishwa na maendeleo ya haraka yaliyofikiwa katika nchi mbalimbali dunia, kutokana na mipango sahihi ya maendeleo ya kiuchumi iliyowekwa na nchi hizo na kusimamiwa kwa utekelezaji. Matukio ya mauaji, vurugu katika uchaguzi mathalani wa Jimbo la Bububu Zanzibar, ni kielelezo tosha cha kuonyesha jinsi gani ukuaji wa demokrasia bado unamashaka makubwa na haki za binadamu kuvunjwa.

Tatizo la umeme nchini;

Hali ya maisha ya Watanzania imeendelea kuwa mbaya, gharama za maisha zinaongezeka na vipato vya wananchi haviongezeki. pamoja na Waziri wa Nishati Na Madini Mhe Prof Muhongo kuwaeleza Watanzania kuwa hakutakuwa na mgao wa umeme na kwamba mgao wa umeme kwa sasa itakuwa ni ndoto, bado maeneo mengi ya nchi yetu ikiwemo jiji la Dar es salaam sote tunashuhudia adha ya kutopata umeme wa uhakika wenye kukatika katika bila utaratibu na ndio kusema kuwa pamekuwepo na mgao usio rasmi unaoendelea. CUF inamtaka waziri wa nishati na madini kuwaeleza Watanzania nini tatizo la msingi juu ya suala la kuendelea kwa mgao wa umeme kinyemela? Aidha, CUF inapinga mpango wowote wa kutaka kuongeza bei ya umeme na badala yake tunaitaka wizara na serikali ya CCM kuona umuhimu wa kuwa na mpango wa uhakika wa kuhakikisha tatizo la umeme linakwisha na watanzania wengi wananufaika na huduma hii kwa gharama zinazoendana na hali za maisha yao.

Kuhusu maliasili ya gesi na mafuta ya petroli na raslimali nyingine, Baraza limetaka Katiba Mpya itamke wazi kuwa hii ni mali ya umma wa Watanzania wote na itatumiwa kwa manufaa ya Watanzania wote. Gesi imepatikana mikoa ya kusini. Mtwara ina bandari asilia. Baraza Kuu limetaka serikali itamke kuwa Mtwara na Lindi itakuwa makao makuu ya sekta ya gesi. Mpango kabambe wa kuandaa miundombinu ya sekta ya gesi uanze kutekelezwa kwa lengo la kuhakikisha viwanda vya saruji, mbolea na kemikali nyingine vinaanzishwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Ni muhimu kuhakikisha kuwa raslimali ya gesi inawanufaisha wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo gesi imepatikana.

Michango ya kujiunga na shule za msingi;

 1. Hivi sasa tupo katika kipindi cha mwisho wa mwaka na wazazi wengi wapo katika harakati za kuwapeleka watoto wao kujiandikisha kujiunga na elimu ya msingi, pamoja na serikali ya CCM kutangaza utoaji wa elimu ya msingi bure, kumekuwepo kwa tatizo kubwa la inayoitwa michango ya uandikishaji watoto kujiunga na darasa la kwanza. michango hiyo inafikia hadi shilingi 50,000 na zaidi katika baadhi ya maeneo. Hili linaweza kuleta athari kubwa kwa wananchi wasio na uwezo kifedha watoto wao wakakosa elimu kujiunga na kupata elimu. Mbali na Naibu waziri wa elimu kulitolea tamko suala hili na kuahidi hatua kali kwa watakao husika na kutoza michango hiyo, inaonekana ni kama kauli ya ‘kisiasa’ zaidi kuliko uhalisia kwani zoezi hilo linaonekana kuendelea katika maeneo mengi ya nchi yetu.

Baraza Kuu linamtaka Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda kuingilia kati suala hili na kuhakikisha kuwa amri ya kutowachangisha wazazi michango hiyo inasimamiwa kwa vitendo watoto wote wenye sifa za kuandikishwa wanaandikishwa bila masharti na vikwazo vyovyote.

Ufisadi wa Kutorosha Fedha nje ya nchi na hasa kwenye mabenki ya Uswizi

 1. Baraza Kuu linaitaka serikali kutumia mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya rushwa na ufisadi kudai fedha zilizotoroshwa nje ya nchi na mafisadi wakubwa zirejeshwe nchini. Serikali itumie sheria ya nchi inayotaka viongozi wa serikali kueleza mali zao ili kuwabana wala rushwa waliotumia wadhifa wao kujipatia utajiri na kutorosha fedha hizo nje ya nchi. Tamko la viongozi wa serikali kuwa wananchi wapeleke ushahidi ni kejeli ya kukwepa kuwajibika. Serikali ndiyo yenye vyombo vya uchunguzi na inaweza kupeleka madai na maombi yake nchi za nje. Serikali inaposhindwa kuchukua hatua zozote ni kielelezo kuwa mfumo wa rushwa na ufisadi umejikita ndani ya serikali yenyewe.

Rushwa ndani ya chaguzi za CCM;

 1. Baraza kuu linalaani vitendo vya rushwa vilivyofanywa na viongozi na wanachama wa CCM na kulalamikiwa pia na baadhi ya viongozi wakuu  wa chama hicho, hasa ukitilia maanani kwamba chama hicho ndicho kilichounda serikali na kipo madarakani. Viongozi wa chama miongoni mwao ndio wanaokwenda kupewa majukumu ya kuongoza idara za serikali, hivyo kuna athari kubwa kiutendaji ndani ya serikali kama kiongozi amepata nafasi hiyo kwa njia ya ufisadi na rushwa. Mfano mdogo unaweza kuthibitishwa ufisadi uliofanwa na viongozi na watendaji wakuu serikali ya CCM kujimilikisha magari yapatayo 974 kwa kuyasajili kwa namba binafsi wakati yakiwa ni magari ya serikali. Baraza kuu linaamini kwamba taarifa hizi za magari ni sehemu ndogo sana katika bahari ya ufisadi yenye kina kirefu katika sekta zote za umma ikiwa ni matokeo ya ufisadi uliosheheni na kujikita ndani ya CCM na serikali zake. ni wazi kuwa CCM ndiyo iliyojenga mfumo wa mtandao huu wa rushwa ambao sasa unawamaliza Watanzania. CUF inatoa wito kwa Watanzania kuwa tusikubali mtandao wa rushwa ulioshinda katika uchaguzi na kushika nafasi nyingi za Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mkutano Mkuu na uongozi wa Jumuiya za CCM haushindi na kukamata dola 2015. Tanzania unahitaji uongozi adilifu wenye dira ya mabadiliko  ili kudhibiti vitendo vya ufisadi, rushwa na kujenga nidhamu na uwajibikaji kwa Taifa.

 

kuhusu mchakato wa ukusanyaji wa maoni katiba;

 1. Tunawapongeza Watanzania wote waliojitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa tume ya kukusanya maoni ya marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ni haki yao ya kikatiba na ni vyema tume ikazingatia maoni hayo ya wananchi. Ni mategemeo ya chama cha CUF na Watanzania kwa ujumla kuwa tume itazingatia maoni hayo kuyaandika katika rasimu ya katiba kabla ya kura ya maoni. Aidha, pamoja na mchakato wa uandikaji wa katiba kwa ujumla wake umepangiwa umalizike katika miezi 18, kipindi hiki hakitoshi kufikia muafaka wa kitaifa kuhusu katiba, kuipitisha katika kura ya maoni, kubadilisha sheria zikidhi mahitaji ya katiba mpya kabla ya kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2014 na uchaguzi mkuu mwaka 2015. Hakuna sababu za msingi za kuharakisha zoezi hili na kupata katiba mbovu isiyokidhi matakwa ya wananchi wenyewe na badala yake tukapata katiba ya matakwa ya watawala.
 2. Baraza Kuu limezingatia kuwa maoni ya katiba yametolewa na wananchi wa pande mbili za Muungano wa nchi zetu wananchi wa Zanzibar na wananchi wa Tanzania bara, ni wazi kuwa pande mbili hizi zimetoa maoni yao kwa kuzingatia haja na matakwa yao kwa wakati tulionao sasa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Tume izingatie maoni ya pande hizo kwa mustakbali wa taifa letu. Masuala yanayohusu MKATABA WA MUUNGANO (Articles of the Union) ni vyema yakaangaliwa upya ili uendane na kukidhi matakwa ya mazingira ya sasa. Tunaitaka tume iweke utaratibu unaofaa katika hatua ya pili ya ukusanyaji wa maoni kwa makundi mbalimbali ya kijamii kwa kuzingatia haki za watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye ulemavu wa usikivu- viziwi. Katiba mpya itakayotokana na wananchi wenyewe, itasaidia sana kujenga DIRA mpya ya mabadiliko makubwa na ya maana kiuchumi, kisiasa na ya muundo wa uendeshaji  wa nchi yetu, ikiongeza kasi ya uwajibikaji wa viongozi.  Hatutarajii tume ya kuratibu ukusanyaji wa maoni ya wananchi juu ya katiba wakajihusisha na kufanya uchakachuaji wa maoni ya wananchi na kutuletea rasimu itokanayo na misimamo na maoni yao binafsi.

 

Umuhimu wa kuwa na TUME HURU YA UCHAGUZI mapema;

 1. Tume ya uchaguzi ina majukumu mengi yanayohitaji muda wa kutosha. Majukumu hayo ni pamoja na kuandikisha wapiga kura wapya, kuandikisha wapiga kura waliopoteza vitambulisho vyao, kuamua na kutekeleza kuwa na vitambulisho vya kura vya biometric kama walivyotumia Ghana katika uchaguzi mkuu wao wa hivi karibuni. Kwa kuwa taratibu zote za kupata katiba mpya na kuitekeleza haziwezi kukamilika kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu, Baraza Kuu linapendekeza maeneo muhimu yanoyohusu uchaguzi ikiwa ni pamoja na mfumo wa uchaguzi, mgombea binafsi na kuwepo kwa Tume huru ya uchaguzi yenye watumishi wake yaamuriwe sasa na kuanza kutekelezwa ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu wa 2015 unakuwa huru na wa haki na usitawaliwe na vurugu, fujo na uvunjifu wa amani.

Matokeo ya Uchaguzi wa Jimbo la Bububu;

 1. Baraza Kuu limepokea taarifa ya uchaguzi wa jimbo la Bububu ambao ulivurugwa kwa makusudi na baadhi ya watendaji wakuu wa serikali ya SMZ, tume ya uchaguzi, vikosi vya SMZ, na JWTZ vilishiriki kikamilifu katika kuhujumu uchaguzi kwa kutumia mtutu wa bunduki kuwatisha wapiga kura wasijitokeze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua muwakilishi wamtakae. Hata hivyo wananchi wa jimbo la Bububu walisimama kidete kutetea haki yao.  Hali hii haionyeshi nia njema ya huko tunakoelekea. Baraza kuu linalaani vitendo hivyo vya uvunjifu wa haki za binaadamu na kuitaka ZEC, serikali ya SMZ, vikosi vya jeshi, kubadilisha fikra zao na kuona kuwa zama zimebadilika.  Vitendo hivi vinatupa tafsiri kuwa zoezi la utoaji wa ajira kwa ubaguzi kunakofanywa na serikali ya SMZ katika vyombo vya ulinzi na usalama  ni ishara tosha ya nia mbaya ya makusudio ya kuendeleza utawala wa mabavu na kukiuka misingi ya demokrasia.  Baraza Kuu linawapongeza wananchi wote waliosimama imara kutetea haki zao pamoja na mgombea wetu wa CUF Mhe. Issa Khamis Issa ambaye amechukua hatua za kisheria kupinga matokeo hayo mahakamani.

 Uchaguzi wa marudio wa madiwani kata 29 Tanzania bara;

 

 1. Baraza Kuu linalaani vurugu na nguvu kubwa iliyotumiwa na vyombo vya dola kukandamiza demokrasia ili kuisaidia CCM ishinde katika kata ya Lwezera, Geita, Mnero, Miembeni, Nachingwea, kata ya Makata wilayani liwale na kitangini wilaya ya newala. Pamoja na mfumo wa demokrasia kuwepo nchini kwa takribani miaka 20 sasa, bado Jeshi la polisi halijaacha mwenendo wake wa awali wa kuingilia uhuru wa wananchi katika kutekeleza haki zao za kikatiba na kutii maagizo ya viongozi wa CCM. Kama Jeshi la polisi halitabadili mwendo huu ni wazi kuwa hata tukiwa na katiba mpya vitendo hivi vitaendelea. Tusingependa kuuingiza nchi yetu kwenye mapambano ya wenyewe tukiamini kuwa hakuna Jeshi linaloweza kupambana na raia wake likashinda hata kama patatokea mauaji ya kiasi gani. Chaguzi za marudio za Jimbo la Bububu na madiwani katika kata 29 imetupa somo la kuanzia sasa kama chama cha siasa lazima tuwe na maandalizi ya kutosha kwa namna zote kuingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2014 na uchaguzi mkuu mwaka 2015 tukiwa NGANGARI KINOMA.

Mwisho;

Baraza kuu linawatakia sikukuu njema ya Noeli na Mwaka Mpya 2013 watanzania wote.

 

 

Haki Sawa Kwa Wote

 

Imetolewa Na;

Baraza Kuu la Uongozi Taifa,                                                                                               Tarehe 23 Disemba, 2012

 

Mh.Julis Mtatiro

Naibu Katibu mkuu Bara

Kwa niaba ya:

 

Mhe. Prof Ibrahim H. Lipumba                                                       Mwenyekiti Wa CUF Taifa.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s