Lipumba:Madai ya Walimu yanalipika

CUF – Chama cha Wananchi kimekuwa kikifuatilia kwa ukaribu matatizo mbalimbali yanayowakumba wafanyakazi na watumishi wa serikali wakiwemo madaktari, walimu na wafanyakazi wa kada zingine

CUF

Mwenyekiti wa CUF Taifa,Prof.Ibrahim Lipumba

.

Hivi karibuni Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kilitangaza mgomo ambao umefanyika kwa siku 3 kabla ya mahakama kuu kitengo cha kazi kuamua shauri la walimu na serikali na kusisitiza kuwa mgomo huo ni batili.

CWT ilitumia kifungu cha 80-(1) (d) cha Sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 kuanza mgomo huo na walimu wanachama wa CWT walianza zoezi la kupiga kura tarehe 25 Julai 2012.

Kwa mujibu wa taarifa baada ya kura zote kupigwa , asilimia 95.7 ya wanachama (walimu) waliunga mkono mgomo, ambao ni walimu wanao fundisha katika shule za awali, msingi, sekondari, maafisa walioko kwenye ukaguzi wa shule za awali, msingi, sekondari, maafisa walioko kwenye ukaguzi wa shule na wakufunzi wa vyuo vya ualimu na maendeleo ya jamii.

Madai makubwa ya walimu na chama chao CWT pamoja na kudai ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho ya kufundishia kwa walimu wa Sayansi asilimia 55, posho ya kufundishia asilimia 50 kwa walimu wa masomo ya  sanaa na posho kwa  walimu wanaoishi katika mazingira magumu.

Ikumbukwe kuwa madai ya walimu ya aina hii na mengine yamedumu kwa zaidi ya muongoz mzima bila kupatiwa dawa. Serikali imekuwa imekuwa ikitoa ahadi nyingi sana za kukamilisha madai na stahiki za walimu bila kutekeleza kwa dhati.

Pamoja na kuwa CUF- Chama Cha Wananchi hakiamini migomo ya wafanyakazi kama suluhisho la kuisha kwa matatizo yao na bila kuingilia maamuzi ya mahakama tunasisitiza kuwa walimu wana madai sahihi, ya haki na yanayopaswa kutekelezwa haraka sana.

Sote ni mashahidi kuwa hali za walimu ni mbaya sana, wanalipwa mishahara kiduchu, wanalipwa posho ndogo ambazo hugeuzwa na kuwa malimbikizo, wanaishi katika nyumba mbovu na wengi wao wamepanga mitaani katika makazi dhaifu, wanafundisha wanafunzi wengi na katika mazingira magumu, walimu ndiyo wamekuwa sehemu ya CCM kujifunzia utawala. CUF Chama cha Wananchi kinawapongeza sana walimu wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya japokuwa hii inayojiita serikali SIKIVU haikuwahi kusikiliza madai yao zaidi ya kutishia kuwafukuza kazi, kuwakamata, kuwashtaki n.k. kama ilivyotokea kwa baadi ya maeneo katika mgomo uliokuwa umeanza mwezi huu kabla mahakama haijangilia kati na kuubatilisha.

 

Mwajiri wa walimu ni rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, chama chetu kilidhani kuwa, rais angelikuja na kauli mahsusi na mpango maalum unaokidhi matatizo yanayowakumba walimu yakiwemo madai ya mambo ya msingi. Badala yake, Rais kikwete akilihutubia taifa kupitia kwa wahariri wa vyombo vya habari katika hotuba yake ya ya mwisho wa mwezi Julai aliyoitoa tarehe 01 Agosti 2012 Ikulu jijini Dar Es Salaam anasema “Madai ya safari hii ni makubwa mno, yametuzidi kimo.  Athari za kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali kutumia asilimia 75 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na kubakiza asilimia 25 kwa kuendeshea Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi.  Haitakuwa sawa.  Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo na wao kusisitiza kugoma.”

Rais anaendelea tena, “Wakati tunaendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili kwa walimu:  Moja, wasiwalazimishe walimu wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na kazi.  Pili,wasitumie watoto isivyostahili kujenga hoja zao.  Nawasihi warudi kwenye meza ya mazungumzo.”

Ukitizama nukuu hizo, zinathibitisha danadana ya serikali ya CCM katika kutekeleza madai ya walimu. Rais hataji serikali yake ina mipango gani na kwa kiasi gani itatekeleza mipango hiyo. Serikali isiyo na mipango kwa vyovyote vile haiwezi kuwatumikia wakulima na wafanyakazi wa nchi yetu. Ni aibu kubwa kwa serikali kuwahadaa walimu kwa mambo yaliyo wazi kabisa.

CUF – Chama Cha Wananchi tunaamini kuwa, kuna fursa nyingi ambazo nchi yetu inazo na ingeweza kuzitumia na kumaliza madai ya walimu na wafanyakazi wengine, likiwapo hili dai kuu la kuongezewa mishahara. Kwa kweli elimu ya Tanzania itaendelea kuwa duni mno ikiwa mchezo huu wa kuwapiga danadana walimu utaendelea. Vigogo wa CCM ambao watoto wao wanasoma katika shule za kimataifa na za kimombo , katu hawawezi kuwafikiria watoto wa masikini wasio na mbele wala nyuma.

Katika utaratibu wa ulipaji mishahara serikalini, TGS A hadi C ni kiwango cha mishahara kwa watumishi wa serikali wanaoanza kazi bila kuwa na shahada ambapo hapa kuna kundi kubwa sana la walimu wa shule za msingi hadi sekondari kwa maana ya wanaofundisha kidato cha 1 hadi cha 4.

Uchambuzi huu hapa chini, unaonesha viwango vya mishahara serikalini kwa mwaka 2011/2012 kwa baadhi ya sekta muhimu ikiwemo elimu, viwango hivi havijahusisha makato ya kodi mbalimbali, ukifanya makato mfanyakazi na hasa mwalimu anabakia na pesa ya kununulia matunda tu.

SEKTA VS TAALUMA CHETI DIPLOMA SHAHADA
UALIMU/ELIMU 244,400 325,700 469,200
AFYA 472,000 682,000 792,200
SHERIA 630,000 871,500 1,000,000

 

Unaweza kujiuliza, kwa nini leo kuna tofauti kubwa sana ya mishahara kati ya sekta moja muhimu ya huduma na nyingine muhimu. Mambo haya yangeshatatuliwa iwapo serikali ya CCM ingekuwa inasema ukweli na kutekeleza ahadi zake. Kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 – 2015, Rais Kikwete  na CCM wanaahidi kuwa; “Serikali kuanzisha mchakato utakaohakikisha kwamba pamoja na kuthamini mchango wa kila mfanyakazi na kufanya kazi katika taaluma zao na kuziheshimu ni muhimu ione tofauti kubwa iliyopo kati ya malipo ya wafanyakazi wa ngazi za juu na wale wa ngazi za chini”.

 

Leo utawala wa Kikwete unaende kumalizika na tofauti ya mishahara bado ni kubwa mno kati ya walimu na kada zingine za wafanyakazi huku Rais akiendelea kuwabembeleza walimu kwa lugha tamu ati serikali yake inawajali.

Kama tunaendelea kuwalipa walimu namna hii, ina maaana ualimu ni wito tu na siyo taaluma kama zilivyo taaluma zingine muhimu, vinginevyo tusishangae kuwa walimu wetu watakuwa mstari wa mbele kuuza bagia na vitumbua shuleni badala ya kufundisha kwa sababu fedha hizo hazilingani kabisa na hali halisi ya maisha.

Ikiwa mwalimu mwenye familia ya watoto wanne mke na wazee wake vikongwe wanamtegemea na ana shahada moja, ukimlipa 469,200 kwa mwezi ina maana kuwa kila mtegemezi asiyeepukika wa mwalimu huyu atatumia tzs 58,625 kwa mwezi na kwa siku kila mwanafamilia atatumia shilingi 1954.16.

Ikiwa tunawafikisha walimu wetu hapo ina maana kuwa hawataweza kujihudumia kimatibabu, kimakazi na huduma zote muhimu hawatazipata, watahudumia matumbo yao tu wakati wote wa kufundisha na watastaafu wakiwa masikini hohehahe, lazima serikali ichukue hatua haraka.

Ni vyema pia mawasiliano kati ya wizara ya elimu na walimu yakaimarishwa ili kujenga mazingira ya wazi ya majadiliano. Mawasiliano yakiimarishwa kati ya wadai na mdaiwa hakuwezi kutokea migomo. Migomo ni uthibitisho wa kuwepo usiri, uzembe, dharau au ubabe. Inasikitisha kwamba mvutano kati ya serikali na walimu hauonyeshi mazingira ya kuaminiana katika kutatua mgogoro husika.

Kukua kwa uchumi wa kisasa wenye uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi kunategemea wafanyakazi wenye ujuzi na maarifa. Kwa hakika utafiti unaonyesha kuwa kukua kwa uchumi wa taifa lolote kunashabihiana kwa karibu na kiwango cha kuwekeza katika sekta ya elimu. Na huwezi kuwekeza katika elimu ikiwa huwalipi walimu kama inavyostahili.

Katika kutilia mkazo elimu ndani ya nchi CUF – Chama Cha Wananchi katika ILANI YA UCHAGUZI YA MWAKA 2010tumesisitiza kuwaSerikali ya CUF itaongeza mishahara ya walimu (katika ngazi zote) ili kukidhi mahitaji yao muhimu. Suala la makazi bora ya mwalimu litakuwa ni jukumu la msingi kabisa la serikali ya CUF ambalo litaanzisha mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za walimu utakaosimamiwa na Serikali kwa haraka ndani ya miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa nchi”.

Pamoja na hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo walimu huku wanaendelea kupata mishahara midogo mno, CCM katika ilani zake za uchaguzi imeendelea kujisifia kwa eti kusimamia elimu kwa uhakika bila kukumbuka kuwa kusimamia mfumo wa elimu ni pamoja na kuwalipa walimu vizuri, ilani ya CCM 2005 – 2010 inajisifia “Mfano mzuri unajitokeza katika sekta ya elimu. Pamoja na mafanikio mengine katika sekta hii, idadi ya wanafunzi wa shule za msingi imeongezeka kutoka milioni tatu na nusu mwaka 1995 na kufikia zaidi ya milioni saba na nusu mwaka 2005. Wakati huo huo wanafunzi wa shule za sekondari wameongezeka zaidi ya maradufu kutoka wanafunzi 190,000 mwaka 1995 hadi wanafunzi 520,000 mwaka wa 2005”

CCM wanasifia idadi ya ongezeko la wanafunzi bila kusema ongezeko hilo litashughulikiwa na walimu wangapi na wao kama serikali wataboreshaje maslahi muhimu ya walimu, huu ni udahifu mkubwa sana.

 

Bila kujua nini wamekifanya katika elimu katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 wanasema, “Katika kipindi cha 2010-2015, CCM itaendelea kuwa karibu na wafanyakazi na kuhakikisha kuwa Serikali zinayatambua na kuyashughulikia kwa ukamilifu na kwa wakati muafaka matatizo yao”.

 

Huu ni mfano mdogo wa ulaghai wa CCM, kwenye ilani ya kutafuta madaraka ya dola wanaahidi kuyatambua na kuyashughulikia madai na matatizo ya wafanyakazi, tena wanasema “tutayashughulikia kikamilifu” lakini leo kero na matatizo ya wafanyakazi vinaonekana kama mzigo mkubwa kwa serikali na inatamka hadharani kuwa “madai ya walimu hayatekelezeki”. CUF – Chama Cha Wananchi tunawashauri walimu watambue kuwa CCM haipo madarakani kutatua matatizo yao, muhimu walimu wakaungana wote ili kuhakikisha CUF inaongoza dola na kuleta mabadiliko makubwa.

 

“Serikali kuanzisha mchakato utakaohakikisha kwamba pamoja na kuthamini mchango wa kila mfanyakazi na kufanya kazi katika taaluma zao na kuziheshimu ni muhimu ione tofauti kubwa iliyopo kati ya malipo ya wafanyakazi wa ngazi za juu na wale wa ngazi za chini”.

 

Migomo ni uthibitisho wa kuwepo usiri, uzembe, dharau au ubabe. Inasikitisha kwamba mvutano kati ya serikali na walimu hauonyeshi mazingira ya kuaminiana katika kutatua mgogoro husika.

 

Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,

Mwenyekiti,

05 Agosti 2012, Dar Es Salaam.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s